Thursday, 29 March 2012

Ushauri kwa Wanawake: Acha Kuomba


Kuchanganyikiwa, Kuumizwa, Kukasirishwa

Hayo ndio maneno yaliyokuwa yanapishana kichwani mwangu wakati nilipokuwa nachukua Biblia yangu ili nianze kuwa na muda wa utulivu na kusali. Nilijisikia kama sina kitu kichwani kwa wakati huo kwani moyo wangu na kichwa changu vilikuwa havikubaliani. Nilikuwa nafikiria jinsi nitakavyobishana na mume wangu juu ya swala Fulani.

Kwanini haoni ninamaanisha nini? Kwanini hanielewi? Kwanini anakuwa msumbufu kiasi hicho?

Nilifunga Biblia yangu na kuamua kuwa jambo la msingi kwa wakati huo ni kupiga magoti na kusali. Hivyo ndivyo wanawake wanaomtumainia Mungu wanavyofanya nilijiambia kichwani mwangu. Na kimoyomoyo nilianza kufikiria orodha ya nini ambacho ningependa Mungu anifanyie kumbadilisha mume wangu kila kitu nilichoona kuwa si sahihi kwa mume wangu kuwa au kufanya. Ghafla nikiwa katikati ya maombi nikaanza kuhisi sauti ya Mungu ikiniambia “Acha”

Acha??? Niache kusali???? Hapo moja kwa moja nikagundua kuwa siyo sauti ya Mungu hivyo nikaendelea kusali. Lakini neno “acha” likaendelea kugonga kichwani kwangu kama mapigo ya moyo wangu yalivyokuwa yanapiga. Kitambo nikaanza kuona lazima kuna kitu si bure na nikagundua ni kwa nini. Mungu hakutaka niwe mke wa “kumbadilisha” mume wangu. Mungu alitaka niwe mke wa “kumpenda” mume wangu.

Nilitaka kuacha kusali, hatimaye nikabadilisha namna ya kusali kwangu. Ni kweli kuna mambo mume wangu alitakiwa kuyafanyia kazi lakini hakuna kizuri kilichotokea kwani muda wote mimi nilikuwa namlaumu kwa madhaifu yake.

Nilihitajika kuwa mwanamke mwenye busara na uthubutu wa kumuomba Mungu aniongoze na kunifundisha jinsi ya kumpenda mume wangu japo ana madhaifu yake. Nilitakiwa nimuulize Mungu ni wapi nakosea, wapi nakuwa mbinafsi ili niweze kufanyia kazi na kujirekebisha.

Nilipobadilisha mwelekeo wangu na kumruhusu Mungu anibadilishe mimi ndipo nilipoona mabadiliko kiasi.

Katika kipindi hiki cha mahangaiko haya Mungu alinifundisha mambo makubwa matatu:-

1. Je haya ni masumbufu au matatizo?

Kuna tofauti kubwa kati ya masumbufu na matatizo. Nilipojua tofauti ya vitu hivyo viwili ilikuwa rahisi kwa mimi kushinda hii vita. Kama haya yalikuwa ni masumbufu inabidi nijitahidi kukubali kubadilika na kukubaliana nayo, mtulivu au kuvumilia.

2. Je ninaomba kwa ajili ya mume au ninamuombea mume?  

Ninapoona kuna kitu kinatakiwa kubadilika kwa mume wangu basi hapo ninatakiwa kumuombea na si kuomba kwa ajili yake. Kuomba kwa ajili yake ni kuonyesha kuwa hupendezwi naye hivyo unataka abadilike. Wakati kumuombea ni kumuomba Mungu atengeneze pale anapoona panahitaji marekebisho. Tunapoomba kwa jina la Mungu tunaomba MAPENZI yake Mungu yatimizwe na kamwe si mapenzi yetu.

3. Mwelekeo wangu uko wapi?

Siwezi kuwa na mamlaka ya kudhibiti mtu fulani kufanya jambo fulani, lakini nina uwezo wa kujidhibiti nisifanye jambo fulani. Mwelekeo wangu hautakiwi kutafuta mwenza/mume aliye mkamilifu bali mwelekeo wangu unatakiwa kuwa mimi niwe mwenza/mke mkamilifu.

Taratibu kadri nilivyoendelea kuondoa moyo wangu kwenye maeneo hayo nimeanza kuona mabadiliko kwenye ndoa yetu. Je bado napata makwazo, nachanganyikiwa, naumia? Bila shaka ndio. Lakini pale nilipoacha kujaribu kumtengeneza au kumbadilisha; nilibadilishwa mimi na kuanza kumpenda jinsi alivyo tena kumpenda kikamilifu kama maandiko yanavyotufundisha katika Waefeso 4:2 Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni ninyi kwa ninyi kwa mapendo

Nimegundua kuwa kumpenda mume wangu ni raha na rahisi sana zaidi ya kujaribu kumtengeneza!!!!

Mwenyezi Mungu, nisaidie kuwa na mwelekeo wa kuwa mke mwema, usiufanye moyo wangu kuwa mgumu. Nisaidie kuziacha fikra zangu na kukusikiliza wewe pale unaponena nami mambo mema yatakayoimarisha ndoa yangu. Katika jina la Yesu ninaomba na kushukuru  Amen

Shukrani kwa rafiki zangu wapenzi Irene Mlola, Lilian Madeje na Evelyn Madeje….. You are the best friends I have in my life. Stay blessed.






No comments:

Post a Comment