Tuesday, 31 January 2012

Wakati Maumivu yanapokusaidia

Je umewahi kukamuliwa jipu? Mungu wangu maumivu yake uliyasikiaje? Lakini nini kilicho na maumivu zaidi? Kubakia na jipu mwilini mwako au kutolewa? Amin amin nakwambia kubakia na jipu mwilini mwako maumivu yake ni makubwa mara dufu. Maumivu makali ya muda mfupi ya kutolewa jipu hukusababishia uhuru wa kudumu. Hii ni sawa sawa na maisha yetu binafsi.

Kila mtu huumia – Kwa njia Fulani, wakati Fulani.  Kwa jinsi tunavyoendelea na maisha yetu ya kila siku, utajikuta umeumizwa na rafiki, ndugu, mfanyakazi mwenzako au hata mtu usiyemfahamu. Baadhi ya majeraha ya haya tunayosababishiwa huwa ni madogo lakini kuna yale ambayo yanaingia ndani yaani ni makali sana yanaweza hata kukuathili kisaikolojia, kiasi cha kukufanya ubuni jeshi la kukulinda kutokana na hayo maumivu. Unaweza ukajikuta umejiingiza kwenye ulevi wa kupindukia, ngono, madawa ya kulevya, ushirikina nk. Hii yote inakuwa ni katika kujijengea himaya ya kutibu yale majeraha yako uliyoyapata. Unaweza kumuachia mtu akusaidie kuyapunguza hayo maumivu bila madhara na kukufanya uwe huru kweli kweli.
Mtu huyu si mwingine bali ni ROHO MTAKATIFU.  Mungu anataka kukuponya na kukufariji na kukufanya usimame imara tena. Biblia inatufundisha kuwa Roho Mtakatifu ni mfariji, mshauri na mponyaji.   Yesu alisema  Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele. (Yohana 14:16) Cha muhimu ni  ni kumruhusu aingie na kumpa nafasi ya kufanya marekebisho na uponyaji wa majeraha yako, na kuwa tayari kufanya yale atakayokwambia ufanye. Inawezekana ni kwa kukaa na na wenzako na kuambizana ukweli, au kwa kuachana na ulevi, ukahaba, au kwa kuamua kusamehe wale wote waliokusababishia majeraha lakini kubwa kabisa ni kwa kusema “ Roho Mtakatifu nakuomba uniponye.”

Kukabiliana na maumivu/ majeraha inaweza kukufanya ujisikie vibaya zaidi kwa muda, lakini baada ya muda fulani itakufanya ujisikie huru. Yesu alisema,“Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32). Je ni maeneo gain unayotaka Mungu ayazungumzie ukweli juu ya maisha yako? Je ni nafsi yako, maisha yako yaliyopita, mustakabali wako?  Chukua muda tafakari na umkaribishe roho wako mtakatifu ili akuponye majeraha yako yote. Muombe akuongoze kwenye uponyaji kamili, anataka kukona ukiwa huru tena!!.

No comments:

Post a Comment